LEO itakuwa siku nyingine ambayo mbabe mmoja kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ataondoka wakati wakali Chelsea watakapovaana na Barcelona.
Tayari PSG, ambao walikuwa wanapewa nafasi kubwa ya kufanya makubwa msimu huu kwenye michuano hiyo wameshaondolewa na Real Madrid wiki iliyopita.
Kati ya Chelsea au Barcelona, leo lazima mmoja aage mashindano hayo makubwa barani Ulaya.
Katika mchezo wa kwanza nchini England, Chelsea walishindwa kulinda ushindi wao na kujikuta wakilazimishwa sare ya bao 1-1 katika Dimba la Stamford Bridge.
Ili Chelsea wafuzu leo wanatakiwa kuhakikisha wanapata ushindi au sare ya mabao 2-2 na kuendelea, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu kwao.
Mara nyingi Barcelona wamekuwa wakishindwa kufanya vizuri ugenini lakini wanaporejea kwenye dimba lao la nyumbani la Camp Nou, hugeuka mbogo.
Chelsea ambao walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita, wanakwenda kwenye mchezo huu wakiwa hawana mafanikio makubwa kwenye ligi hiyo baada ya kuwa katika nafasi ya tano kwenye msimamo.
Huu utakuwa mchezo mwingine ambao staa wa Barcelona, Lionel Messi, atataka kuonyesha tena umwamba wake baada ya kuifunga Chelsea kwenye mchezo uliopita ikiwa ni mara yake ya kwanza anafanya hivyo baada ya timu hizo kukutana mara nane na yeye akiwemo.
Messi ambaye ni kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Hispania, anataka kuonyesha tena uwezo wake leo kwenye dimba la nyumbani.
“Tumejiandaa kupambana, tumejiandaa kwa kuwa tunafahamu kuwa tunakutana na timu bora kwenye ulimwengu huu wa soka, hatujiamini kwa kuwa kila kitu kwetu kipo kwenye mpangilio na tunafahamu lolote linaweza kutokea,” anasema beki wa Barcelona, Thomas Vermaelen.
Barcelona na Chelsea zimeshakutana mara 13 na mara tano kati ya hizo ni hatua ya mtoano, hali inayoonyesha kuwa ni timu zinazojuana.
Kama leo Barcelona itafanikiwa kufuzu robo fainali, basi itakuwa mara yao ya 11 mfululizo inatua kwenye hatua hiyo, hivyo Chelsea wenyewe wakitaka ushindi kwa nguvu kubwa kwa kuwa wamefuzu hatua hiyo mara moja tu kati ya miaka mitano iliyopita.
Hata hivyo, rekodi hii haimpi hata mmoja nafasi ya kutinga robo fainali kwa kuwa kati ya mara 13 ambazo timu hizo zimekutana, Chelsea wameshinda mara nne, Barcelona mara tatu na mara sita zimetoka sare, takwimu ambazo zinaufanya mchezo huu kuwa wazi sana.
Hata hivyo, Barcelona wanakwenda kwenye mchezo huu wakiwa hawajapoteza mchezo wowote wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya 24 ya hivi karibuni waliyocheza nyumbani, hii ikiwa ni kuanzia Septemba 2013, wameshinda michezo 22 na kutoka sare miwili tu.
Katika sare hizo walitoka na Atlético Madrid na Juventus.
Rekodi ya timu za England kwa Barcelona siyo nzuri ikiwa timu hiyo imefanikiwa kushinda michezo 19 imetoka sare mara 11 na kupoteza michezo miwili tu, jambo ambalo ni hatari kwa Chelsea leo.
Wakati hawa wakiwa hivi Chelsea wenyewe hawajafungwa kwenye michezo kumi waliyocheza nchini Hispania, wameshinda michezo mitatu na kutoka sare saba.
Hata hivyo, wameonekana kuwa na matokeo mazuri kila wanapotoka sare nyumbani kwa kuwa kati ya michezo sita minne walifanikiwa kupata ushindi ugenini.
“Tunafahamu kinachotupeleka Barcelona, tunafahamu kuwa kama tukifungwa basi tutaondoka na kama tukipata suluhu tunaondoka, jambo tunalotakiwa kufanya ni kuhakikisha kwanza tunapata bao.
“Kufunga bao kwenye mchezo huu ndiyo njia pekee ambayo inaweza kutusaidia sisi kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu kwa hatua inayofuata, lakini kama tukianza kufungwa sisi ina maana kuwa tutatakiwa kufanya kazi kubwa sana.
“Napafahamu Camp Nou kwa kuwa ni sehemu niliyokaa kwa muda, najua hali inavyokuwa kwenye uwanja ule kama Barcelona wanatakiwa kushinda, hauwezi kuwa mchezo rahisi kwetu hata kidogo, lazima tupambane sana,” anasema mshambuliaji wa Chelsea, Pedro.
0 Comments